Kama inavyoeleweka Watanzania wengi kipato chao ni kidogo, hivyo sio rahisi kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku kama chakula, mavazi , elimu, huduma za afya nk.
Ahadi nyingi zimekuwa zikitolewa na viongozi na wabunge wakati wa campaign za uchaguzi na shughuli mbalimbali za kijamii. Lakini viongozi na wabunge hao wakitoka maeneo husika na kuwapa visogo wananchi wenye shida, wanasahau hata kutimiza ahadi zao.
Tunaelewa jinsi viongozi na wabunge wanavyolipwa mishahara mizuri, wanavyoishi kwenye nyumba nzuri zenye generator za dharura kukabiliana na tatizo la mgao wa umeme, na wanavyotembelea magari ya kifahari kuwawezesha kufika popote wanapohitaji nk. Lakini ukiangalia walipa kodi hali ni kinyime na kusikitisha!
Tumeshuhudia jinsi viongozi wanavyopelekwa kutibiwa nje ya nchi, huku maelezo yakitolewa kwamba taratibu huwa zinafuatwa kutekeleza hilo! Sio kosa la wakubwa ama viongozi hao kutibiwa nje ya nchi bali ni mfumo uliowekwa na serikali ndio kikwazo. Sio siri kwani mifano mizuri ni Mwl Nyerere alitibiwa nje ya nchi siku za mwisho, pia muda si mrefu Malecela na sasa Dr Mwakyembe (Naibu Waziri wa Ujenzi) amepelekwa India kwa matibatu. Je mfumo wa huduma za afya nchini unatatizo gani na serikali inafikiria nini?
Walipa kodi wengi ambao ni masikini awana uwezo wa kugaramia matibabu nje ya nchi, tunasoma maombi ya michango kwenye blogs na vyombo mbalimbali vya habari ya kuwasaidia wenye shida kupata matibabu. Swali ni kwamba serikali inakuwa wapi mpaka raia waombe misaada? Kwanini serikali ya Tanzania isiwajibike kwa kuweka utaratibu mzuri kuwawezesha viongozi na wananchi wote kupata matibabu ndani ama nje ya nchi bila kubagua? Iweje walipa kodi wateseke na kupoteza maisha kwa kukosa matibabu wakati viongozi wanaenda kutibiwa nje ya nchi?
Bila walipa kodi wenye afya nzuri serikali aitapata kodi kuendesha nchi, na nchi inahitaji viongozi bora wenye afya nzuri kuongoza nchi. Hivyo serikali inahitaji kutoa ufafanuzi kuhusu upatikanaji wa matibabu nje ya nchi, la sivyo wasio na uwezo na viongozi wote watibiwe ndani ya nchi jambo litakalo lazimisha kuwekeza katika huduma hizo hapa nchini na kutoa ajira kwa raia badala ya kupoteza fedha za kigeni kulipia matibabu nje ya nchi, na kuokoa maisha ya wasio na uwezo.
No comments:
Post a Comment